Bila shaka umewahi kusikia neno ngekewa, kama bado basi fahamu ya kuwa ngekewa ni mnyama mdogo mwenye wingi wa mambo ambayo unapaswa kufahamu.
Chapisho hili moja kwa moja linaangazia kwa uchache juu ya mambo mbalimbali kuhusu mnyama huyu na imani za watu zilizojengeka juu ya mnyama huyu.
Kwanza kabisa, inakadiriwa kuwa huko south America ndiko kunakopatikana kwa wingi ngekewa wakubwa ambao hufikia uzito wa takribani kg 91, kwa lugha ya kimombo ngekewa huitwa capybara unafahamu hili?
Jusfan fact tovuti maarufu katika chapisho maalumu kuhusu mnyama ngekewa inaeleza kuwa mnyama huyu ni mnyama anaependwa zaidi na upendo huo husababishwa na yeye mwenyewe kujipenda.
Katika makazi yao , ngekewa hukaa katika makundi kuanzia ngekewa 10-20 . Lakini ngekewa mmoja anaposafiri husindikizwa na kundi la viumbe wengine ikiwemo wanyama na ndege. Kinachoshangaza ni kuwa wanyama na viumbe wengine hupenda sana kuwa karibu na ngekewa jee ni kwanini?
Karibu karne zote zilizopita duniani kote jamii nyingi zinaamini kuwa kuna uhusiano wa karibu sana kati ya wanyama, mimea, wadudu na ndege . Ni katika uhusiano huo binaadamu hupata dawa na kitoweo cha kila siku ili kusogeza maisha.
Ni katika kutaka kukabiliana na mazingira yake binaadamu alibuni hili na lile na alichoona kuwa ni bora alikiboresha, basi ni katika hitaji la kujikinga na kujitibu maradhi binaadamu alibuni dawa kutoka kwa wanyama na mimea, lakini kwa jamii za kiafrika mambo ya dawa mara nyingi sana hufata misingi ya imani fulani zilizojengeka.
Kwa nchini Tanzania kuna jamii nyingi ya watu inayoweka imani kubwa kwa mnyama ngekewa na uwezo wa kupata bahati, mvuto, kupendwa na watu na pia kupata utajiri.
Jamii ya watu wa nyanda za juu kusini na kanda ya ziwa inaamini kuwa ;
Kama utabahatika kupata majani ya alipokuwa amelala mnyama ngekewa kisha ukachanganya na madawa mengine basi utakuwa mtu mwenye kupendwa sana na watu, kusikilizwa na hata kuwa na bahati.
Kuna baadhi ya watu wanaoamini kuwa ukifanikiwa kupata manyoya ya ngekewa na kuyachoma kisha ukachanganya na madawa mengine ukioga au kupaka pamoja na mafuta basi utaongoza kwa kuvutia watu , kupendwa, na kutoa kila aina ya mkosi.
Hawakuishia hapo , kuna wengine wanaamini kuwa kama utapita njia aliyopita ngekewa basi hakuna jambo utakalolifanya kisha lisifanikiwe, utakuwa ni mtu mwenye kufuatwa na watu katika mambo yako , utakuwa na wingi wa wafuasi na vibaraka.
Jee uliwahi kusikia haya yote?
Inaelezwa kuwa baadhi ya watu fulani fulani ikiwemo wasanii na wafanyabiashara wanaongoza kwa kumtumia mnyama huyu kuboresha mambo yao ikiwemo kukubalika na hata kujizolea ushawishi katika jamii.
Jee wewe ulisikia nini kuhusu mnyama ngekewa na uliwahi kumuona wapi ? Basi tuandikie maoni yako katika kurasa zetu .