Nilivyokula Nyama Ya Kobe Ni Tamu .
Simulizi ya kweli kabisa kutoka kwa kijana Abubakar Othman Mzee wa mkoani Kigoma namna alivyokula nyama ya kobe akijua kuwa ni nyama ya bata.
" Tulipotoka Tanzania kwenda nchini Congo kutafuta dawa za kienyeji misitu ya huko Congo sikuwa nimewahi hata kujaribu kula kobe, sikujuwa kuwa kumbe safari yangu ya Congo ingesababisha mimi kula kobe..." Abubakar anazungumza huku akivuta kumbukumbu.
Mwaka 2021 Abubakar akiambatana na kaka yake mganga wa kienyeji mkoani Kigoma walifunga safari hadi misitu ya nchini Congo kwenda kutafuta dawa za miti shamba kwaajili ya kiringe chao cha uganga.
Baada ya safari ndefu Abubakar, kaka yake Omari na wenzao wengine watatu wanafanikiwa kuingia Congo na kufikia kwa mwenyeji wao , siku ya kwanza, ya pili kisha ya tatu inakatika wakiendelea kusaka dawa katika mapori ya Congo. Siku moja majira ya jioni Abubakar anawaaga wenzie na kwenda matembezi mafupi kijiji jirani kutoka pale walipofikia.
Na huko Abubakar anakutana na vijana watano waliouzunguka moto wakipeana zamu kuchochea kuni huku wakiendelea kuigeuza geuza nyama iliyokuwa ikiendelea kuuzima moto kwa mafuta mengi, na hapo Abubakar anajipenyeza na kushiriki zoezi, nyama inaiva na taratibu Abubakar anatupia vipande mdomoni mwake bila kuuliza ni nyama ya nini.
" Tuliendelea kula bila mimi kujua ni nyama ya nini na bahati mbaya sikuuliza mapema mpaka pale mmoja katika wale watoto aliponiuliza kwani na kwenu huko mnakula kobe? hapo ndio nikafahamu ... "
Baada ya kutafuna kobe kisawasawa Abubakar aliamua kuondoka na kurudi kundini kwa wenzie huku akiapa kuifanya siri yake bila kumwambia mtu yeyote, kwa bahati mbaya sana kobe aliemla alisababisha mzio kwenye mwili wake na kumsababishia mabaka mikononi mwake na hapo Abubakar alitoboa siri kwa wenzie.
" Ilibidi niseme ukweli sasa, maana nilitoka mabaka karibu mikono yote huku mwili ukiwasha sana, ndio nikamwambia yule mwenyeji wetu na siku ile ile upesi upesi kuna dawa ya miti shamba aliniandalia na kunambia nioge na nyingine ninywe... "
Safari ya kurudi Tanzania iliwadia huku Abubakar akisalia na vitu viwili kichwani mwake, moja ni ladha ya nyama ya kobe akifikiri kuwa ni bata na pili ni nguvu ya dawa za asili katika matibabu ya allergy. Kwako msomaji uliwahi kula kitu gani cha ajabu ukidhani ni nyama nono?